Mwalimu Isaacks Manyonyi- Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Uhuru wa Dini (South Nyanza Conference) |
Agizo la utume la injili ni kuwaendea na kuwafundisha mataifa yote kama alivyoagiza Mwokozi Yesu Kristo. Elimu kwa ajili ya umilele ni sehemu ya njozi na wajibu wa kanisa letu kumshirikisha kila mmoja wetu kuanzia katika familia, shule za makanisa na makanisa kwa ujumla.
Hebu fikiria wewe ni Muisrael, na hakika wewe ni Muisrael wa kiroho, punde tu mmepewa amri kumi kutoka kwenye mikono ya Mungu mwenyewe. Wiki chache zijazo mtakuwa mkiingia katika nchi ya ahadi inayomwagika maziwa na asali. Fikiria nini kitatokea upande wa pili, ng'ambo ya mto Jordan. Kule ng'ambo ya mto kuna watu wapagani ambao hata hawamjui Mungu, kuna umizimu na ushenzi tupu.
Unapoiendea nchi ya ahadi si tu kwamba inatoa maziwa na asali,la hasha, nchi hiyo itatoa damu pia. Kule unaweza kupoteza maisha yako, safari hii si lelemama, unapaswa kujipanga kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizoko mbele yako. Tamaduni za kishezi za upande ule zinatishia upendo wako kwa Mungu. Utafanyaje kuwasaidia watoto wako wabaki kuwa watiifu na imara kwa Mungu?
- Lazima tuwafundishe: Mungu ametuachia siri ya kuwaachia watoto wetu maadili ya dini. Wazazi wote ni walimu, sisi sote ni walimu. Wapo wanaodhani jukumu hili ni la watu fulani; wanakosea sana!!!!. Zoezi hili la ufundishaji ni la mzunguko,Watoto , wanafunzi wetu wafundishwe sheria za Mungu nyumbani, shuleni, kanisani na hatimaye nyumbani tena.
- Kila mzazi anawajibika kumpatia mtoto wake elimu ambayo itampatia ufahamu- kumjua Bwana Mungu na kuwa mbebaji wa huduma takatifu.
- Wazazi kuwa kilelezo,mfano ni mbinu ya kipekee sana ambayo Mungu ametupatia kuwafundisha watoto wetu kwa ajili ya umilele. Kama mzazi, mwalimu na kiongozi inatupasa kuishi maisha ambayo tunataka watoto wetu waishi. fanya matembezi unayotaka watoto wako watembee, ongea maongezi unayotaka waongee. Utafiti unaonyesha kuwa kwa kadri mzazi unavyojishughulisha, kujihusisha na mambo ya kiroho, shughuli za kanisa, watoto nao watakuwa 'active' katika programu za kanisa Wakorintho 13:5
- Zoezi la kuelimisha watoto kwa ajili ya umilele halitafikiwa kama wazazi watakosa muda wa kukaa na watoto wetu. Wazazi wengi hawana muda wa kuwa watoto wao, huondoka mapema alfajiri kwenda kazini, ofisini katika biashara zao, safarini n.k na kurudi usiku. Ninapendekeza njia zifuatazo, kwa ajili ya kuhakikisha kuwa tunafundisha watoto wetu kwa bidii kwa ajili ya umilele.
- Unapoendesha gari, mkiwa pamoja na watoto wako tumia muda huo kuwafundisha, kuwakumbusha sheria za Mungu, maisha matakatifu na maisha ya umilele.
- Mnapoangalia television/luninga, tumia dakika kadhaa kwa kuzima luninga na kufundisha na kuelezea upendo wa Mungu.
- Kaa na watoto wako kanisani, wanaona uaminifu wako unapotoa zaka na sadaka. Waambie namna Mungu anavyokupenda/anavyowapenda na kuwabariki.
- Peleka watoto wako katika shule za kanisa, maana watajengwa vizuri kitaaluma, kitabia lakini pia watapewa elimu kwa ajili ya umilele.
- Unapoongea na mtoto wako kwa njia ya simu, msisaliamiane tu na kutuma 'pocket money' bali agana nae kwa kumkumbusha sheria za Mungu.
- Usiache kuwakusanya watoto wako katika maombi ya asubuhi mnapoamka na jioni/usiku kabla ya kulala kwa kuwafundisha neno la Mungu.
- Siku ya sabato,fanya matembezi ya asili 'nature walk' na watoto wako, ili waone mkono wa Mungu kwa vile wanavyoviona.
- Wanapofanya mambo mema, wapongeze ikiwezekana wazawadie. Usiwe mzazi wa kutoa adhabu tu wakati wanapokosea na ukapotezea kuwapongeza wakati wanapofanya vizuri.
- Mwalimu mwaadventista unapofundisha darasani, kabla hujaanza somo, katikati ya somo, mwisho wa somo kumbuka unafundisha kwa ajili ya umilele. Uwe kielelezo kwa wanafunzi unaofundisha.
Bwana atusamehe pale tuliposahau jukumu letu kama wazazi na walimu. Tulipewa muda na hatukuutumia ipasavyo. Tumepewa watoto na wanafunzi hatukuonyesha bidii katika kuwaadibisha na kukuza imani zao.
Tunafanya agano jipya na Mungu wetu kuwafundisha watoto wetu kwa bidii kwa ajili ya umilele.
MUNGU AKUBARIKI
Post a Comment