Home » » "TUMJUWEJE MUNGU?" Pr. ROBERT TUVAKO

"TUMJUWEJE MUNGU?" Pr. ROBERT TUVAKO

Written By SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH on Sunday, July 30, 2017 | July 30, 2017

Mchungaji Robert Tuvako- Marketing Officer Ufunuo Publishing House


Mchungaji anayesimamia kufasiri na masoko ya vitabu kutoka "Ufunuo Publishing House' Mchungaji Robert Tuvako kutoka Morogoro amehubiri wakati wa ibada ya jioni ya mkutano wa makambi ulioanza tarehe 29 Julai 2017 katika viwanja vya Kanisa la Waadventista wa Sabato Kirumba-Mwanza. Soma hapa chini hubiri lake nalo limeanza kama ifuatavyo:

Kwa nini ni muhimu kumjua Mungu? Kwa nini tualike rafiki zetu waje kanisani? Je tunaweza kukaa tu na Mungu akajidhihirisha kwetu bila kumtafuta? Katika Yohana 17:3 inasisitiza kumjua Mungu kwa kila Mwanadamu. 

Kwa wakazi wa Mwanza na Tanzania nzima, wanakumbuka ajali ya Treni iliyotokea mwaka 1996 ambayo iligharimu maisha ya watanzania wengi. Je ulishawahi kupata taarifa ambayo ilikata mawasiliano yako? na hata walionena karibu yako huwezi kuwasikia kwa sababu ya taarifa hiyo?.
Katika Biblia Takatifu kuanzia Aya ya 13 ya Luka 24 inawataja vijana wawili ambao walikuwa wakisafiri kutoka Yerusalemu wakienda Emau. Ilikuwa ni kama maili 8 kati ya miji hii miwili. Wakiwa wanatembea walikuwa wakijadiliana kuhusu kifo cha Yesu ambacho kimetokea siku 3 tu zilizopita. Walikuwa wanalia (Mjumbe wa Mungu Ellen G White anasema walikuwa wamezingwa na huzuni na wakichuruzika machozi kiasi kwamba walikuwa hawawezi kusikia ya pembeni).

Biblia takatifu inasema, Macho ya vijana hawa wawili yalikuwa yamefumbwa. Wakati huo kama zilikuwepo Televisheni na whatsapp au Youtube na Facebook za nyakati hizo ni hakika taarifa za kifo cha Yesu zilikuwa zimeenea katika pande zote za mji. Wote katika Israeli walikuwa na taarifa ya kifo cha Yesu. Bwana Yesu akiwa ameambatana nao hawa vijana wawili, anauliza kana kwamba hajui taarifa hiyo ya kifo cha Yesu. (Mungu wetu anapouliza huwa anauliza kwa lengo la kuvuta usikivu wa Mungu. Hata katika Bustani ya Edeni alimuuliza Adamu kana kwamba hajui walichokuwa wamekitenda.)

Mwandishi anasema Yesu alipowaona akina Cleopa wanahuzunika, Yesu alitamani kuwafuta machozi lakini kwa kujua shina la matatizo ya vijana wawili (Kukata tamaa) aliaanza kuwafundisha ili wamuelewe. Wakasimama wakiwa wamekunja nyuso zao, naye Cleopa akiwa ndiye mnenaji mkuu kuliko mwenzake ambaye Biblia haijamtaja jina lake alimuuliza Yesu kwa kushangaa kuwa ni mtu wa ajabu ambaye hata hajui taarifa za Kifo cha Yesu. Naye Yesu alimjibu “Mambo gani?”. Katika aya ya 19 wakamjibu Yesu kuwa ni mambo ya Yesu wa Nazareti.
Angalia kitenzi kilichotumika “aliyekuwa nabii…..nasi tulikuwa naye…..” kwa kauli hii vijana hawa wanaonesha kuwa tumaini lao kwa Yesu lilikwisha siku ile ile ya Ijumaa ambayo yesu Kristo alikufa pale msalabani. Marafiki hawa wa Yesu walisahau ahadi ya Yesu kuwa atafufuka siku ya tatu. 

Je kwa leo, ile Imani yako ya zamani imepoa? Je changamoto za maisha zimekukatisha tamaa?. Nawaambieni hii hali naifananisha na 'Watu wazima na afya zao wakipoteza matumaini wanaweza kunywa sumu kuliko mgonjwa aliye kitandani ambaye ana tumaini'. 

Aya ya 25 inazungumzia jinsi ufufuo wa Yesu ulivyotendeka, na habari njema ya wahubiri wa habari ya ufufuo wa Yesu walikuwa wanawake. Neno la Mungu linasema Yesu akawaambia “Enyi wenye mioyo migumu kiimani…” Ikimaanisha Yesu Kristo akiwaambia vijana hawa wawili 'nikiwa nanyi, wewe Cleopa na wenzako, mlikuja wakati nikihubiri injili ya torati,mlishuhudia miujiza yangu, niliwafundisha torati na leo hamna hata ile imani ya ufufuo wa Kristo? lo!'. 

Aya ya 26, 'Je haikumpasa Kristo kuingia katika mateso haya?' Kristo alianza kuwafundisha kwa kuanza na maswali kwa wale wanafunzi wawili wa Yesu. Alianza kuwapa muhtasari wa maisha ya Yesu. Biblia haituambii alitemnbea nao kwa muda gani, Biblia inatuambia aliwapa muhtasari wa ujumbe wa Mungu.

Aya ya 28, Yesu alijifanya kana kwamba anataka kuendelea na safari. Ulikuwa ni utamaduni wa Kiebrania wa kumbembeleza mgeni, katika aya ya 29 inasema wakamshawishi Yesu. Ukarimu ni tabia. Ndipo Yesu alikubali na kuingia nao.

Katika aya ya 30. Nalitegemea kuona mambo matano na nitapenda tuyahesabu kwa pamoja; 1. Alitwaa mkate, 2. akaubariki, 3. akaumega, 4. akawapa. Jambo la tano nilitegemea kusikia kuwa walikula. La hasha hawakula ule mkate. Aya ya 31 inasema macho yao yakafumbuka. Alifanya mambo 4 tu kati ya mambo matano. Hebu fikiria mtu aliyekufa, mara ghafla unamuona ukiwa naye mezani baada ya kubariki chakula, hakika hautakula chakula hicho. Ni hakika Vijana wale wawili hawakula chakula kile baada ya macho kufumbuliwa bali walitoka mbio kurudi Yerusalemu.

Kwa nini Yesu hakuwafumbua macho yao wale vijana wawili? Kwa nini aliwafumbua macho yao mara baada ya mafundisho ya muda mrefu? Kwa nini hakuwafumbua macho yao katikati ya  njia? Yesu hakuwafumbua macho yao kwa sababu hataki kanisa lake kwenda kwa MISUSUMIKO. Yesu anataka kanisa liende kwa maandiko ya Mungu. Anataka kanisa linalosoma maandiko ya Mungu. Wanaosoma neno la Mungu watafumbuliwa macho yao. Wanaosubiri kuja kwa Yesu kwa mara ya pili ni wale kila siku wanasoma maandiko matakatifu.

La muhimu ni neno la Mungu ndani ya mioyo yetu. Kumjua Mungu kutakamilishwa na neno la Mungu kukaa ndani ya mioyo yetu ili kuzaa nia njema ya kumwabudu Mungu. Torati ya neno la Mungu ikae ndani yetu.

BWANA AWABARIKI
Share this article :

+ comments + 1 comments

31 May 2020 at 09:03

Ubarikiwe Mchungaji Tuvako kwa ujumbe mzuri

Post a Comment

 
Need Support? Contact : Creating Website and Blog | Stanley Isaac Manyonyi | Twitter
Copyright © 2017. SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger