Home » » SHINYANGA ADVENTIST SECONDARY SCHOOL KUANZA JANUARI 2018

SHINYANGA ADVENTIST SECONDARY SCHOOL KUANZA JANUARI 2018

Written By SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH on Tuesday, April 11, 2017 | April 11, 2017

Mchungaji Sadock Butoke (President South Nyanza Conference)
Ndoto iliyootwa miaka kadhaa iliyopita ya kuanza kwa shule ya sekondari ya Shinyanga kuanzia mwezi Januari 2018, shule itakayomilikiwa na kanisa la Waadventista wa Sabato, ndoto ambayo ilisubiriwa kwa muda kutekelezwa, leo mwenyekiti wa jimbo la kusini mwa Ziwa Viktoria, mchungaji Sadock Butoke ameongoza wanasemina waliohudhuria mafunzo ya kutengeneza matofali yatokanayo na udongo na saruji, kwa pamoja wamechimba na kuanza ujenzi wa msingi wa jengo la utawala. Jengo la utawala litakuwa na ofisi ya mkuu wa shule, ofisi ya makamu wa mkuu wa shule, ofisi ya walimu, ofisi ya katibu muhtasi na stoo.

Mchungaji Sadock Butoke
Wakati wa ujenzi wa msingi wa jengo la utawala, mchungaji Butoke amesema lengo la kuja Shinyanga ni kuhamasisha jamii wa Shinyanga kupata shule ya Sekondari itakayokuwa na uwezo wa kutoa elimu kwa jamii ya Shinyanga."Tumekuja hapa kwa lengo la kutengeneza matofali ambayo ni ya gharama nafuu ambayo yanapatikana kwa kuchanganya udongo na saruji. Kwa kawaida mfuko mmoja wa saruji unatoa matofali kati ya 100-120. Wazo hili lilikuja kwa sababu katika 'conference' hii tuna miradi mingi inayohusiana na ujenzi. Hapa Shinyanga tunajenga sekondari ya Shinyanga 'Shinyanga Adventist Secondary School', tunajenga sekondari ya Nkome, lakini pia kule Itilima tunajenga shule ya msingi"  alisema Mchungaji Butoke.

Mchungaji Sadock Butoke
Sambamba na hilo kila mtaa katika jimbo la kusini mwa Ziwa umeagizwa kujenga nyumba za wachungaji. Kwa hiyo elimu ya utengenezaji wa matofali ya udongo na saruji umetoa matokeo chanya kwa watu waliohudhuria maana wanasemina wamekaririwa wakishuhudia kuwa mara baada ya mafunzo watanunua mashine kwa lengo la kufyatua matofali na kutumia ujuzi kwa manufaa ya jamii, kanisa na wao binafsi.

Pamoja na mafunzo ya utengenezaji wa matofali, katika mwanzo huu uongozi wa kanisa jimbo la kusini mwa ziwa Viktoria wameamua kuanza ujenzi wa ofisi za watumishi wa shule yaani 'admistration block'. Kwa hiyo mafunzo ya utengenezaji wa matofali yatazalisha matofali yatakayotumika kujenga boma la jengo la utawala mara baada ya ujenzi wa msingi wa jengo la utawala kukamilika.

Mwalimu Isaacks Manyonyi
Naye Mkurugenzi wa Elimu na Uhuru wa dini jimbo la kusini mwa ziwa viktoria mwalimu Isaacks Manyonyi amekaririwa akisema, "tunategemea shule hii ya Shinyanga Adventist Secondary School kuanza Januari 2018, tayari vyumba vinne na ofisi moja vimekwishajengwa, na kazi ya ujenzi wa jengo la utawala inaendelea. Tunamshukuru Mungu kazi inaendelea maana vifaa vipo, matofali yanaendelea kutengenezwa kwa nguvu kazi ya vijana na washiriki wa kanisa wanaojitoa kwa hali na mali. Tuna imani ile njozi ya kuanza kwa shule Januari 2018, kwa uwezo wake Mungu itatimia hii njozi."

Mchungaji Kilinda
Wachungaji kutoka mitaa mbalimbali walihudhuria katika mafunzo na uanzishwaji wa ujenzi wa jengo la utawala. Mchungaji wa mtaa wa Shinyanga Mjini ambaye ndiye alikuwa mwenyeji wa mafunzo haya, Mchungaji J. kilinda amewashukuru sana uongozi wa Jimbo la Kusini mwa ziwa Viktoria kuja kuhamasisha ujenzi wa shule ya sekondari Shinyanga. Pia alitoa wito kwa wana Shinyanga kuwa wasimamizi wakuu wa ujenzi wa Shule hii kwa kuiona ni fursa kwa wana Shinyanga."Jengo hili ambalo limeanzishwa na fedha za wana ATAPE "Association Of Tanzania Adventist Professionals and Entrepreneurs" katika mkutano wa mwaka 2013 ambapo mgeni rasmi alikuwa mchungaji David Mmbaga pale Lubaga na moja ya fedha zilizosaidia hapa ni Tshs Milioni 2 zilizochangwa wakati huo. Kwa hiyo namshukuru Mungu ndoto ya siku nyingi leo imeanza kutekelezeka. Hii ndiyo shule tunayoweza kujivunia kwa kuwa ndiyo shule yetu itakayotuunganisha. Ninaomba wadau wa elimu, wajasiriamali, washiriki mmoja mmoja kujitoa kwa hali na mali ili kutimiza njozi ya shule hii kuanza Januari 2018" alisema Mchungaji Kilinda.

Mzee Kanakoko
Naye mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa shule hii, mzee Deonatus Kanakoko alisema kuwa kuna msisimko mpya unaoenda kutimiza ndoto ya uanzishwa wa shule. Aliomba wana Shinyanga kuchangia ujenzi wa shule na kuhakikisha njozi inatimia ili vijana wa wana Shinyanga wapate mahali pa kusoma kwa elimu bora ya duniani na mbinguni wakiwa hapa hapa Shinyanga.

Aliyevaa kofia ni Mchungaji Kilinda(Mchungaji wa Mtaa wa Shinyanga Mjini na mhazini wa mtaa ndugu Tumaini Nduta
Mhazini wa kanda ya Shinyanga ndugu Tumaini Nduta alikariri akisema washiriki waendelee kutoa michango yao na aliwahakikishia usalama wa fedha zote zitakazochangwa kuwa zitatumika vizuri kukamilisha mradi wa ujenzi wa shule. Alitoa mfano wa utunzaji wa fedha za ATAPE ambazo zilichangwa kuanzia mwaka 2013 kuwa hadi leo mwaka 2017 zilitunzwa na kusubiri uendelezwaji wa ujenzi wa shule bila kubadili matumizi ya fedha hizo.

Kutoka kushoto ni Mzee Kanakoko(mwenyekiti kamati ya ujenzi wa shule), Mwalimu Isaacks Manyonyi(Mkurugenzi wa Elimu-South Nyanza Conference), ndugu Kisinga (Makamu wa Mchungaji-Mtaa wa Ushirika) na wanasemina wakibeba tofali na kuzipeleka katika eneo la ujenzi wa msingi wa jengo la utawala


Mafundi akiendelea na ujenzi wa msingi wa jengo la utawala


Share this article :

Post a Comment

 
Need Support? Contact : Creating Website and Blog | Stanley Isaac Manyonyi | Twitter
Copyright © 2017. SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger