Jumapili ya Julai 2, 2017 zaidi ya wanachama wa chama cha Watafuta Njia ( Path Finder-PF) wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Shinyanga Mjini, wamefanya matembezi ya zaidi ya umbali wa Kilometa 5 kwa lengo la kujifunza ukakamavu ikiwemo kupata ujuzi wa utambuzi wa alama mbnalimbali zinazotumika katika mawasiliano ya matembezi. PF hao wakiwa katika vikosi vitatu vilivyokuwa chini ya viongozi wao walianza matembezi yao kuanzia kanisani kuelekea katika eneo la mkutano ambalo lipo katika uwanja wa Shule ya Sekondari Ibinzamata wakipitia msitu wenye miti mbalimbali iliyopo kata ya Ndala Mjini Shinyanga.
Kwa mara kadhaa vikosi vyote vitatu vilipotea njia lakini baadae mara baada ya kurudia kusoma alama walizofundishwa waliweza kusahihisha makosa yao na kuweza kukamilisha safari yao iliyoanza majira ya saa 3 asubuhi na ilipotimia saa 7 mchana walifika salama katika eneo la mwisho ambapo waliweza kupumzika na kutoa taarifa ya safari yao.
Pamoja na kujifunza stadi za ukakamavu pia, katika eneo hilo la mkutano lililokuwa limezungukwa na miti mingi ya miembe, PF walishuhudia kilimo cha bustani iliyokuwa katika hatua ya uandaaji wa matuta ya bustani kwa ajili ya upandaji wa mboga za majani ikiwemo mchicha, matikiti maji, spinachi na chinese. Mmiliki wa eneo hilo ambaye ndiye aliyekuwa akiandaa matuta ya bustani alikubali kuzungumza na PF, na ametoa wito kwa PF kuwa na ujuzi wa kutengeneza bustani zao katika maeneo yao ya nyumbani ili ziweze kupunguza gharama za kununua mboga za majani na viungo vya mboga katika familia zao. Pia amesema kuwa iwapo watajihusisha na kazi ya kutengeneza bustani zao, watapata maarifa ya kupenda kufanya kazi ambazo Mungu atawabariki katika kazi zao ikiwemo kuwa na akili katika masomo yao na baadae kuwa raia wema kwa Taifa na hata katika ufalme wa Mbinguni.
Wakati huo Mkurugenzi wa PF Kanisani ndugu Peter Stima amewaeleza PF kuwa matembezi waliyoyafanya ni sehemu ya mtaala wao ili waweze kuhitimu kwa ajili ya kutunukiwa nishani mbalimbali zinazotambulika katika kanisa la Waadventista wa Sabato Duniani katika mkutano wa Vijana utakaofanyika mwezi Desemba katika mkoa wa Iringa.
Baadae vijana wa PF walicheza mpira wa miguu kwa wavulana na pia wasichana walicheza mpira wa pete katika viwanja vya shule ya sekondari Ibinzamata na ilipofika saa 11 jioni walirejea Kanisani Shinyanga Mjini na kurudi katika makazi yao wakiwa salama.
Post a Comment