Kisa cha kwanza: Palikuwepo na mfungwa mmoja
aliulizwa, “Chakula cha mwisho unachopenda kula ni kipi? Na wakati huo kamera
ziliendelea kuonyesha tukio hilo. Aliagiza alichopenda na camera ziliendelea
kuonyesha akila chakula hicho na wakati huo huo tena kamera zilihamia kwa
familia zilizoathirika na matendo mabaya ya mfungwa huyu na vile vile kamera
ilihamia kuonyesha familia ya mfungwa huyu. Cha ajabu kauli yake ya mwisho
haikuwa na majuto bali aliendelea kusisitiza kuwa alitenda hayo yote kwa
makusudi.
Kisa cha pili: Costen Fleming mwenye miaka 75,
aliugua kwa kupasuka mishipa ya damu na aliambiwa kuwa hatapona. Aliambiwa
unataka nini kabla hujafa? Huyu aliomba sigara na wine
Leo ukiambia unataka nini kabla ya kufa utaomba nini? Na sasa
ninanena na wewe unayesoma ujumbe huu, ungekuwa wewe ungeomba nini? Unavyojenga moyo wako ndivyo unavyojenga
tabia yako, na hicho kilicho katika moyo wako ndicho kitaonekana mara ya mwisho
katika wakati wako wa mwisho. Ukubwa wa tabia unaweza kuonekana hata katika dakika ya mwisho.
Kamwe sio bure kuhudhuria mikutano ya kiroho. Kiini cha somo
kinapatikana katika aya 13 ya 2 Timotheo 4, ambapo tunasoma Mtume Paulo
anamwandikia Timotheo, na hii ndio sura
ya mwisho ya mtume Paulo aliyoandika na kana kwamba Mtume Paulo alijua
ndio mwisho wake. Tunajifunza kuwa ulikuwa ni wakati za mwisho kwa mtume Paulo na
alianza kwa kuagiza kazi zilizo katika moyo wake.
Paulo aliyekuwa Sauli alikuwa mtu maarufu sana, mwenye uwezo,
alikuwa akiheshimika sana, na ni tajiri sana. Na Yesu alipokutana naye hakuwa
peke yake katika msafara wake maana alikuwa ni mtu mashuhuri sana katika jamii
yake.
Lakini Yesu alipomtawala
Paulo, Paulo alianza kugawa kila utajiri aliokuwa nao. Na wimbo wake
ulikuwa ni injili ya Yesu. Na alipokuwa gerezani aliagiza vitu viwili tu,
Hakuagiza dhahabu wala almasi.
Kwaya ya Kanisa la Waadventista wa Sabato Kirumba-Mwanza wakiimba wakati wa Ibada
Mara kadhaa Imani yetu
haifanani kama tulivyokuja kwa Yesu, maana tupo tunaokuja kwa Yesu tukiwa ni
maarufu na wakati Fulani wengine twaja tukiwa maskini. Vyovyote tunavyokuja,
kwa mali au kwa umaskini, iwe kwa hadhi au dharau, ninapenda kutoa wito kwako mpendwa umalize wito wako wa hapa
duniani na Yesu Kristo. Ni heri makombo Yesu Kristo kuliko keki za Shetani.
Ombi la kwanza ni Joho.
Kwa nini Paulo aliomba Joho? Tazama Paulo yuko kwenye shimo gerezani, kuna baridi kali
sana katika shimo hilo ambalo lina unyevu kila wakati. Wakati alipokamatwa,
alimpa Karpo vitu viwili ili visije vikapotea, alimpa joho na vitabu. Katika
gereza Paulo hana hata mtu wa kumuomba joho. Aliagiza joho lake. “kilicho chako kina thamani kuliko vya
wengine”.
Sijui kama mimi na wewe kama tungepewa fursa ya kuagiza sijui
tungeagiza nini? Paulo aliagiza Joho lake, alijua kwamba hata kama atakufa,
mwili wake utakuwa umefunikwa na joho lake. Ndiye aliyeandika kuwa mwili huu ni
hekalu la Mungu. Aliendelea kuwajibika katika mwili wake.
Ombi la pili ni vitabu.
Kwa nini vitabu? Kwa
ulimwengu wa sasa katika basin a usafiri mwingine wengi utawakuta wana simu
wakichati. Lakini pia katika karne iliyopita katika magari ya abiria, tuliwashuhudia
watu wakizungumza. Na katika nchi za magharibi utakuwa wasafiri wengi wanasoma
vitabu mbalimbali wakiwa ndani ya vyombo vyao vya usafiri.
Mpendwa msomaji, napenda kuwapatia ujumbe huu kuwa, Kando ya
torati, Mtume Paulo alipenda kusoma vitabu vingine (Matendo 17:28 “Kwa maana
ndani yake tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu,
mtunga mashairi alivyosema, maana sisi sote tu wazao wake”)
Paulo anamwandikia Timotheo kuomba mambo makuu mawili na hasa
jambo la pili kwa sababu anajua kuwa atakaponyongwa atakuwa amemwachia ujumbe
kuwa bila kusoma vitabu, kanisa litapata utapiamlo. Changamoto zetu ni
kufundishana kupitia usomaji wa vitabu. Sisemi kusoma tu kesha la asubuhi, bali
ninachomaanisha ni usomaji wa vitabu wa kutafuta hekima ya mbinguni ipambanuayo
mambo kwa hekima kuu. Bwana anataka kanisa linalosoma. Heri asomaye.
BWANA AKUBARIKI
Post a Comment