Home » » RAIS MAGUFULI AABUDU NA WASABATO MAGOMENI

RAIS MAGUFULI AABUDU NA WASABATO MAGOMENI

Written By SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH on Saturday, September 02, 2017 | September 02, 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli ameungana na waumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato kusali Ibada ya Sabato katika kanisa la Waadventista wa Sabato Magomeni jijini Dar es Salaam. Rais Magufuli ameambatana na mkewe katika ibada ya leo ambayo imeongozwa na Mchungaji Mark Warwa Malekana ambaye ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania.
 Rais Joseph Pombe Magufuli na Mkewe Janeth Magufuli katika Ibada ya Sabato pamoja na waumini wengine ndani ya kanisa la Waadventista wa Sabato Magomeni.(Picha kwa hisani ya Stephen Letta)

Katika ibada hiyo mchungaji Malekana amemshukuru Rais Magufuli kwa kuungana na waumini wa kanisa la Waadventista wa sabato katika Ibada ya Sabato na baadaye alimuombea Rais na taifa kwa ujumla. "Kiongozi anayetawala watu kwa haki, akitawala kwa kicho cha Mungu, atakuwa kama jua la asubuhi. mheshimiwa Rais, Mungu akufanye jua la asubuhi, asubuhi nyeupe, angavu na isiyo na mawingu, tunamuomba Mungu atimize ahadi hii ya utumishi kwa kiongozi wetu Rais John Pombe Magufuli". Amesema Mchungaji Malekana.

Ujumbe mkuu ambao mchungaji Malekana amewataka waumini wote kuufuata ulijengwa katika kisa cha mtumishi wa Mungu Yusufu alipokuwa Misri kama kiongozi aliyeikomboa nchi ya Misri kutokana na baa la njaa kali iliyoikumba dunia kwa miaka saba. Amesema kuwa Tanzania ya leo inawataka waumini kuwa kama Yusufu ili kuisaidia Serikali ya Tanzania katika kufikia malengo iliyojipangia.

Mara baada ya Ibada kuu, Rais Magufuli amelipongeza Kanisa la Waadventista wa Sabato kwa huduma za kiroho ambalo kanisa linatoa ikiwemo pia huduma za kijamii kama vile afya na elimu. Rais Magufuli amelihakikishia kanisa kuwa Serikali yake inatambua mchango wa kanisa katika maeneo mbalimbali ya nchi na kuahidi kuendelea kushirikiana na madhehebu yote katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.
 Rais Magufuli (Kushoto) akimsikiliza Dkt. Jim Yonaz ambaye ni mmoja wa waumini wa kanisa la Waadventista wa Sabato Magomeni pia ni Mhariri Mkuu wa Magazeti ya Serikali (TSN). Katikati ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania,Mch.Mark Warwa Malekana.(Picha kwa hisani ya Stephen Letta)

Pamoja na kushiriki ibada ya sabato, Rais amechangia kiasi cha shilingi milioni 5 na mifuko ya saruji 400 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa kanisa jipya ambalo kanisa la Magomeni linajenga. Juma ya shilingi milioni 25.3 zimepatikana baada ya mheshimiwa Rais Magufuli kuendesha harambee ya papo kwa papo ya kuchangia ujenzi wa kanisa jipya. Rais amesema kuwa sio mara yake ya kwanza kuabudu katika kanisa la waadventista wa Sabato, amekuwa akiabudu wakati akisoma chuo kikuu cha Dar es Salaam katika sikukuu ya vibanda (Makambi) na makongamano mbalimbali ya Wasabato.
Rais Joseph Pombe Magufuli akisalimiana na mtoto aliyehudhuria ibada ya Sabato. (Picha kwa hisani ya Stephen Letta)


Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Mbariki Rais Joseph Pombe Magufuli
Share this article :

Post a Comment

 
Need Support? Contact : Creating Website and Blog | Stanley Isaac Manyonyi | Twitter
Copyright © 2017. SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger