Home » » KILA MUUMINI AHUSIKE KUBORESHA ELIMU YA KIADVENTISTA

KILA MUUMINI AHUSIKE KUBORESHA ELIMU YA KIADVENTISTA

Written By SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH on Saturday, April 08, 2017 | April 08, 2017

Dr. Mashauri Mjema- Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na uhuru wa Dini (North Tanzania Union Conference)
Fungu Kuu: "Kaeni ndani yangu,nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi msipokaa ndani yangu." Yohana 15:4

Mwelekeo wa kanisa la Waadventista wa Sabato katika miaka hii mitano ni kuweka kipaumbele katika utume. Msisitizo mkubwa umewekwa kwenye eneo la kumfanya kila muumini wa kanisa ahusike moja kwa moja katika uinjilisti. Kwa kufanya mambo matatu muhimu kutasaidia kufikia lengo. Mambo hayo ni; moja ni kufanya juhudi kumfikia Mungu, pili ni kuwafikia wengine tukiwa na Mungu na tatu ni kuifikia jamii tukiwa na Mungu. Mambo hayo matatu yakifanywa kwa ukamilifu, yatagusa maeneo ya elimu ya kiadventista ambayo ni roho, mwili, akili na jamii.

Katika eneo la kumfikia Mungu kila mzazi, mlezi au mwalimu, ni lazima afanye juhudi za makusudi kumtafuta Mungu wa mbinguni. Huu ni msingi wa mambo yote yatakayofuata. Katika kukua kiroho ni lazima kutenga muda maalumu wa kutafakari na kujifunza neno la Mungu kwa njia ya usomaji wa Biblia, lesoni, vitabu vya roho ya unabii na machapisho mengine unaoambatana na maombi.(Zaburi 119:105, 2Timotheo 3:16)

Mahusiano kati ya mlezi wa mtoto na Mungu yanapokuwa mazuri, msingi imara wa malezi utakuwa umejengwa. Hili litafungua njia ya kumjengea mtoto msingi ambao ulishajengeka tayari kwa anayemfundisha. Biblia inasema "Je Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa doa yake? kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya" Yeremia 13:23. Mtu ambaye hawezi kujibadili mwenyewe au kubadilishwa, je ataweza kumbadilisha mwingine? Kujisalimisha na kunyenyekea kwa Mungu ni jambo la kwanza kabla ya kumbadilisha mwingine. Sasa hatua hii mzazi aweza kumjengea mtoto tabia ya kusoma neno la Mungu.

Eneo la pili ni kuwafikia wengine tukiwa na Mungu kwa mzazi, mlezi au mwalimu kuwa mfano kwa kuhudhuria mikutano yote ya kiroho kanisani, shuleni au chuoni. Umoja na ushirikiano ni vema ukahimizwa kwa watoto na vijana wetu. Makanisa au taasisi ambazo jumuia zao hazikutani mara kwa mara ushirikiano wao huwa na kasoro.

Eneo la tatu ni kuifikia jamii tukiwa na Mungu. Kila muumini ana wajibu wa kuijali jamii kwa njia mbalimbali. kila mmoja anaweza kushiriki moja kwa moja katika mahubiri ya hadhara, kushuhudia nyumba kwa nyumba na kugawa vitabu na magazeti. Wajibu wake mwingine ni kuwajulisha majirani na watu anaowashuhudia kuhusu elimu ya kiadventista na taasisi zetu za elimu.






Share this article :

Post a Comment

 
Need Support? Contact : Creating Website and Blog | Stanley Isaac Manyonyi | Twitter
Copyright © 2017. SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger