Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mheshimiwa Josephine Matiro leo amelipongeza kanisa la Waadventista wa Sabato kwa kukarabati jengo moja lenye vyumba sita katika kambi ya kuwalelea wazee Kolandoto Manispaa ya Shinyanga. Mkuu wa Wilaya amesema kanisa limefanya kazi nzuri ya kujali wazee ambao wanakabiliwa na changamoto ya kuishi katika majengo ambayo yana hali mbaya kiasi cha kuhatarisha maisha ya wazee hao.
"Ninapenda kutoa wito kwa wadau wengine mbalimbali kujitolea kama kanisa la Wasabato walivyofanya ili kuweza kuwatatulia changamoto mbalimbali hawa wazee wetu ikiwemo hii ya kukarabati majengo mengine yaliyobaki". Alisema Josephine Matiro
Kabla ya kukabidhiwa jengo hilo, mkuu wa Wilaya alikubali mwaliko wa kuhudhuria ibada ya Sabato ya leo ambayo iliongozwa na Mwenyekiti wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Jimbo Kuu Kaskazini mwa Tanzania Dr. Godwin Lekundayo ambaye aliambata na Mwenyekiti wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Jimbo la Kusini mwa Ziwa Nyanza Mchungaji Butoke na Mkurugenzi wa Elimu wa Jimbo la Kusini mwa Ziwa Nyanza Mwalimu Isaacks Manyonyi.
Naye Dr. Godwin Lekundayo akisoma neno la Mungu wakati wa kukabidhi jengo hilo, amesema kuwa dini safi ni ile inayojali na kuwahudumia wahitaji ambayo iliwagusa kanisa kupitia idara yake ya vijana kuguswa na kuamua kuwasaidia wazee walioko katika kambi ya wazee Kolandoto kwa kuwakarabatia jengo ili waweze kuishi kwa usalama. "Huduma hii sio ya mwisho, tutaendelea kutoa huduma kwa wazee hawa zaidi na zaidi kwa kadri neno la Mungu linavyotuelekeza kutenda". Alisema Dr Lekundayo.
Dr Godwin Lekundayo akisoma neno katika Biblia Takatifu wakati wa kukabidhi jengo lililokarabatiwa na Kanisa la Waadventista wa Sabato Kanda ya Shinyanga kupitia Idara ya Vijana (Picha zote kwa hisani ya Malunde Blog)
Sambamba na kukabidhi jengo hilo lililogharimu kiasi cha shilingi milioni 1.8, kanisa la Waadventista wa Sabato kanda ya Shinyanga limetoa zawadi ya vitabu vya injili, mafuta ya kupikia, boksi la sabuni ya kufulia, mbuzi mmoja na mchele kilo 120.
Mkuu wa Wilaya akikabidhi zawadi ya chakula kwa msimamizi wa kituo (Picha zote kwa hisani ya Malunde Blog)
Post a Comment