Latest Post

WAVUMBUZI WAPEWA MAFUNZO YA TUZO YA VYOMBO VYA HABARI NA MAWASILIANO

Written By SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH on Sunday, June 05, 2022 | June 05, 2022

Wanachama wa chama cha wavumbuzi wakiwa darasani 

Wanachama wa chama cha wavumbuzi katika kanisa la Waadventist wa Sabato Shinyanga Mjini, wamehudhuria katika mafunnzo ambapo wamejifunza masuala mbalimbali yanayohusu vyombo vya habari na mawasiliano.

Katika mafunzo hayo wavumbuzi hao ambao ni watoto wenye umri usiozidi miaka 10, wamejifunza kuwa vyombo vya habari ni aina ya mawasiliano ambayo uhusisha magazeti, televisheni, redio, majarida, vitabu, mikanda ya video na mitandao ya kijamii kuwezesha mawasiliano yenye lengo la kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi.



Pia wavumbuzi hao wamejifunza baadhi ya matumizi ya vyombo vya habari na mawasiliano ikiwemo kutumika katika utoaji wa habari muhimu, kutangaza biashara ili kukuza uchumi, kuelimisha jamii na kutangaza injili, kukuza mahusiano katika jamii.

Katika hali iliyovutia zaidi ni wavumbuzi waliweza kuorodhesha hasara za vyombo vya habari na mawasiliano kama vile upotevu wa maadili kwa kuangalia vipindi na taarifa ambazo zina maadili machafu, pia vyombo vya habari vinachangia watu kukosa muda wa kusoma na kutafakari neno la Mungu ikiwa ni pamoja kujenga tabia ya uvivu na uzembe kwa kutumia muda mwingi kuangalia television.

Wanachama wa chama cha wavumbuzi wakiwa darasani 

Mwisho wa mafunzo, wavumbuzi walipata wasaa wa kusoma neno la Mungu katika kitabu cha Wafilipi 4:8 ambapo wavumbuzi waliona kanuni ya kutazama, kuona na kusikiliza vyombo vya habari ambavyo vina ujumbe ulio msafi, ujumbe wenye adabu, wenye staha na wenye sifa njema.

RAIS MAGUFULI AABUDU NA WASABATO MAGOMENI

Written By SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH on Saturday, September 02, 2017 | September 02, 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli ameungana na waumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato kusali Ibada ya Sabato katika kanisa la Waadventista wa Sabato Magomeni jijini Dar es Salaam. Rais Magufuli ameambatana na mkewe katika ibada ya leo ambayo imeongozwa na Mchungaji Mark Warwa Malekana ambaye ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania.
 Rais Joseph Pombe Magufuli na Mkewe Janeth Magufuli katika Ibada ya Sabato pamoja na waumini wengine ndani ya kanisa la Waadventista wa Sabato Magomeni.(Picha kwa hisani ya Stephen Letta)

Katika ibada hiyo mchungaji Malekana amemshukuru Rais Magufuli kwa kuungana na waumini wa kanisa la Waadventista wa sabato katika Ibada ya Sabato na baadaye alimuombea Rais na taifa kwa ujumla. "Kiongozi anayetawala watu kwa haki, akitawala kwa kicho cha Mungu, atakuwa kama jua la asubuhi. mheshimiwa Rais, Mungu akufanye jua la asubuhi, asubuhi nyeupe, angavu na isiyo na mawingu, tunamuomba Mungu atimize ahadi hii ya utumishi kwa kiongozi wetu Rais John Pombe Magufuli". Amesema Mchungaji Malekana.

Ujumbe mkuu ambao mchungaji Malekana amewataka waumini wote kuufuata ulijengwa katika kisa cha mtumishi wa Mungu Yusufu alipokuwa Misri kama kiongozi aliyeikomboa nchi ya Misri kutokana na baa la njaa kali iliyoikumba dunia kwa miaka saba. Amesema kuwa Tanzania ya leo inawataka waumini kuwa kama Yusufu ili kuisaidia Serikali ya Tanzania katika kufikia malengo iliyojipangia.

Mara baada ya Ibada kuu, Rais Magufuli amelipongeza Kanisa la Waadventista wa Sabato kwa huduma za kiroho ambalo kanisa linatoa ikiwemo pia huduma za kijamii kama vile afya na elimu. Rais Magufuli amelihakikishia kanisa kuwa Serikali yake inatambua mchango wa kanisa katika maeneo mbalimbali ya nchi na kuahidi kuendelea kushirikiana na madhehebu yote katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.
 Rais Magufuli (Kushoto) akimsikiliza Dkt. Jim Yonaz ambaye ni mmoja wa waumini wa kanisa la Waadventista wa Sabato Magomeni pia ni Mhariri Mkuu wa Magazeti ya Serikali (TSN). Katikati ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania,Mch.Mark Warwa Malekana.(Picha kwa hisani ya Stephen Letta)

Pamoja na kushiriki ibada ya sabato, Rais amechangia kiasi cha shilingi milioni 5 na mifuko ya saruji 400 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa kanisa jipya ambalo kanisa la Magomeni linajenga. Juma ya shilingi milioni 25.3 zimepatikana baada ya mheshimiwa Rais Magufuli kuendesha harambee ya papo kwa papo ya kuchangia ujenzi wa kanisa jipya. Rais amesema kuwa sio mara yake ya kwanza kuabudu katika kanisa la waadventista wa Sabato, amekuwa akiabudu wakati akisoma chuo kikuu cha Dar es Salaam katika sikukuu ya vibanda (Makambi) na makongamano mbalimbali ya Wasabato.
Rais Joseph Pombe Magufuli akisalimiana na mtoto aliyehudhuria ibada ya Sabato. (Picha kwa hisani ya Stephen Letta)


Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Mbariki Rais Joseph Pombe Magufuli

"BILA KUSOMA VITABU, KANISA LITAPATA UTAPIAMLO" PR. ROBERT TUVAKO

Written By SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH on Monday, July 31, 2017 | July 31, 2017


Kisa cha kwanza: Palikuwepo na mfungwa mmoja aliulizwa, “Chakula cha mwisho unachopenda kula ni kipi? Na wakati huo kamera ziliendelea kuonyesha tukio hilo. Aliagiza alichopenda na camera ziliendelea kuonyesha akila chakula hicho na wakati huo huo tena kamera zilihamia kwa familia zilizoathirika na matendo mabaya ya mfungwa huyu na vile vile kamera ilihamia kuonyesha familia ya mfungwa huyu. Cha ajabu kauli yake ya mwisho haikuwa na majuto bali aliendelea kusisitiza kuwa alitenda hayo yote kwa makusudi.

Kisa cha pili: Costen Fleming mwenye miaka 75, aliugua kwa kupasuka mishipa ya damu na aliambiwa kuwa hatapona. Aliambiwa unataka nini kabla hujafa? Huyu aliomba sigara na wine

Leo ukiambia unataka nini kabla ya kufa utaomba nini? Na sasa ninanena na wewe unayesoma ujumbe huu, ungekuwa wewe ungeomba nini? Unavyojenga moyo wako ndivyo unavyojenga tabia yako, na hicho kilicho katika moyo wako ndicho kitaonekana mara ya mwisho katika wakati wako wa mwisho. Ukubwa wa tabia unaweza kuonekana hata katika  dakika ya mwisho.

Kamwe sio bure kuhudhuria mikutano ya kiroho. Kiini cha somo kinapatikana katika aya 13 ya 2 Timotheo 4, ambapo tunasoma Mtume Paulo anamwandikia Timotheo, na hii ndio sura  ya mwisho ya mtume Paulo aliyoandika na kana kwamba Mtume Paulo alijua ndio mwisho wake. Tunajifunza kuwa ulikuwa ni wakati za mwisho kwa mtume Paulo na alianza kwa kuagiza kazi zilizo katika moyo wake. 

Paulo aliyekuwa Sauli alikuwa mtu maarufu sana, mwenye uwezo, alikuwa akiheshimika sana, na ni tajiri sana. Na Yesu alipokutana naye hakuwa peke yake katika msafara wake maana alikuwa ni mtu mashuhuri sana katika jamii yake.
Lakini Yesu alipomtawala  Paulo, Paulo alianza kugawa kila utajiri aliokuwa nao. Na wimbo wake ulikuwa ni injili ya Yesu. Na alipokuwa gerezani aliagiza vitu viwili tu, Hakuagiza dhahabu wala almasi.
 Kwaya ya Kanisa la Waadventista wa Sabato Kirumba-Mwanza wakiimba wakati wa Ibada

Mara kadhaa Imani yetu haifanani kama tulivyokuja kwa Yesu, maana tupo tunaokuja kwa Yesu tukiwa ni maarufu na wakati Fulani wengine twaja tukiwa maskini. Vyovyote tunavyokuja, kwa mali au kwa umaskini, iwe kwa hadhi au dharau, ninapenda kutoa  wito kwako mpendwa umalize wito wako wa hapa duniani na Yesu Kristo. Ni heri makombo Yesu Kristo kuliko keki za Shetani.

Ombi la kwanza ni Joho. Kwa nini Paulo aliomba Joho? Tazama Paulo yuko kwenye shimo gerezani, kuna baridi kali sana katika shimo hilo ambalo lina unyevu kila wakati. Wakati alipokamatwa, alimpa Karpo vitu viwili ili visije vikapotea, alimpa joho na vitabu. Katika gereza Paulo hana hata mtu wa kumuomba joho. Aliagiza joho lake. “kilicho chako kina thamani kuliko vya wengine”.

Sijui kama mimi na wewe kama tungepewa fursa ya kuagiza sijui tungeagiza nini? Paulo aliagiza Joho lake, alijua kwamba hata kama atakufa, mwili wake utakuwa umefunikwa na joho lake. Ndiye aliyeandika kuwa mwili huu ni hekalu la Mungu. Aliendelea kuwajibika katika mwili wake.

Ombi la pili ni vitabu. Kwa nini vitabu? Kwa ulimwengu wa sasa katika basin a usafiri mwingine wengi utawakuta wana simu wakichati. Lakini pia katika karne iliyopita katika magari ya abiria, tuliwashuhudia watu wakizungumza. Na katika nchi za magharibi utakuwa wasafiri wengi wanasoma vitabu mbalimbali wakiwa ndani ya vyombo vyao vya usafiri.
Mpendwa msomaji, napenda kuwapatia ujumbe huu kuwa, Kando ya torati, Mtume Paulo alipenda kusoma vitabu vingine (Matendo 17:28 “Kwa maana ndani yake tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, maana sisi sote tu wazao wake”)

Paulo anamwandikia Timotheo kuomba mambo makuu mawili na hasa jambo la pili kwa sababu anajua kuwa atakaponyongwa atakuwa amemwachia ujumbe kuwa bila kusoma vitabu, kanisa litapata utapiamlo. Changamoto zetu ni kufundishana kupitia usomaji wa vitabu. Sisemi kusoma tu kesha la asubuhi, bali ninachomaanisha ni usomaji wa vitabu wa kutafuta hekima ya mbinguni ipambanuayo mambo kwa hekima kuu. Bwana anataka kanisa linalosoma. Heri asomaye. 

BWANA AKUBARIKI

"TUMJUWEJE MUNGU?" Pr. ROBERT TUVAKO

Written By SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH on Sunday, July 30, 2017 | July 30, 2017

Mchungaji Robert Tuvako- Marketing Officer Ufunuo Publishing House


Mchungaji anayesimamia kufasiri na masoko ya vitabu kutoka "Ufunuo Publishing House' Mchungaji Robert Tuvako kutoka Morogoro amehubiri wakati wa ibada ya jioni ya mkutano wa makambi ulioanza tarehe 29 Julai 2017 katika viwanja vya Kanisa la Waadventista wa Sabato Kirumba-Mwanza. Soma hapa chini hubiri lake nalo limeanza kama ifuatavyo:

Kwa nini ni muhimu kumjua Mungu? Kwa nini tualike rafiki zetu waje kanisani? Je tunaweza kukaa tu na Mungu akajidhihirisha kwetu bila kumtafuta? Katika Yohana 17:3 inasisitiza kumjua Mungu kwa kila Mwanadamu. 

Kwa wakazi wa Mwanza na Tanzania nzima, wanakumbuka ajali ya Treni iliyotokea mwaka 1996 ambayo iligharimu maisha ya watanzania wengi. Je ulishawahi kupata taarifa ambayo ilikata mawasiliano yako? na hata walionena karibu yako huwezi kuwasikia kwa sababu ya taarifa hiyo?.
Katika Biblia Takatifu kuanzia Aya ya 13 ya Luka 24 inawataja vijana wawili ambao walikuwa wakisafiri kutoka Yerusalemu wakienda Emau. Ilikuwa ni kama maili 8 kati ya miji hii miwili. Wakiwa wanatembea walikuwa wakijadiliana kuhusu kifo cha Yesu ambacho kimetokea siku 3 tu zilizopita. Walikuwa wanalia (Mjumbe wa Mungu Ellen G White anasema walikuwa wamezingwa na huzuni na wakichuruzika machozi kiasi kwamba walikuwa hawawezi kusikia ya pembeni).

Biblia takatifu inasema, Macho ya vijana hawa wawili yalikuwa yamefumbwa. Wakati huo kama zilikuwepo Televisheni na whatsapp au Youtube na Facebook za nyakati hizo ni hakika taarifa za kifo cha Yesu zilikuwa zimeenea katika pande zote za mji. Wote katika Israeli walikuwa na taarifa ya kifo cha Yesu. Bwana Yesu akiwa ameambatana nao hawa vijana wawili, anauliza kana kwamba hajui taarifa hiyo ya kifo cha Yesu. (Mungu wetu anapouliza huwa anauliza kwa lengo la kuvuta usikivu wa Mungu. Hata katika Bustani ya Edeni alimuuliza Adamu kana kwamba hajui walichokuwa wamekitenda.)

Mwandishi anasema Yesu alipowaona akina Cleopa wanahuzunika, Yesu alitamani kuwafuta machozi lakini kwa kujua shina la matatizo ya vijana wawili (Kukata tamaa) aliaanza kuwafundisha ili wamuelewe. Wakasimama wakiwa wamekunja nyuso zao, naye Cleopa akiwa ndiye mnenaji mkuu kuliko mwenzake ambaye Biblia haijamtaja jina lake alimuuliza Yesu kwa kushangaa kuwa ni mtu wa ajabu ambaye hata hajui taarifa za Kifo cha Yesu. Naye Yesu alimjibu “Mambo gani?”. Katika aya ya 19 wakamjibu Yesu kuwa ni mambo ya Yesu wa Nazareti.
Angalia kitenzi kilichotumika “aliyekuwa nabii…..nasi tulikuwa naye…..” kwa kauli hii vijana hawa wanaonesha kuwa tumaini lao kwa Yesu lilikwisha siku ile ile ya Ijumaa ambayo yesu Kristo alikufa pale msalabani. Marafiki hawa wa Yesu walisahau ahadi ya Yesu kuwa atafufuka siku ya tatu. 

Je kwa leo, ile Imani yako ya zamani imepoa? Je changamoto za maisha zimekukatisha tamaa?. Nawaambieni hii hali naifananisha na 'Watu wazima na afya zao wakipoteza matumaini wanaweza kunywa sumu kuliko mgonjwa aliye kitandani ambaye ana tumaini'. 

Aya ya 25 inazungumzia jinsi ufufuo wa Yesu ulivyotendeka, na habari njema ya wahubiri wa habari ya ufufuo wa Yesu walikuwa wanawake. Neno la Mungu linasema Yesu akawaambia “Enyi wenye mioyo migumu kiimani…” Ikimaanisha Yesu Kristo akiwaambia vijana hawa wawili 'nikiwa nanyi, wewe Cleopa na wenzako, mlikuja wakati nikihubiri injili ya torati,mlishuhudia miujiza yangu, niliwafundisha torati na leo hamna hata ile imani ya ufufuo wa Kristo? lo!'. 

Aya ya 26, 'Je haikumpasa Kristo kuingia katika mateso haya?' Kristo alianza kuwafundisha kwa kuanza na maswali kwa wale wanafunzi wawili wa Yesu. Alianza kuwapa muhtasari wa maisha ya Yesu. Biblia haituambii alitemnbea nao kwa muda gani, Biblia inatuambia aliwapa muhtasari wa ujumbe wa Mungu.

Aya ya 28, Yesu alijifanya kana kwamba anataka kuendelea na safari. Ulikuwa ni utamaduni wa Kiebrania wa kumbembeleza mgeni, katika aya ya 29 inasema wakamshawishi Yesu. Ukarimu ni tabia. Ndipo Yesu alikubali na kuingia nao.

Katika aya ya 30. Nalitegemea kuona mambo matano na nitapenda tuyahesabu kwa pamoja; 1. Alitwaa mkate, 2. akaubariki, 3. akaumega, 4. akawapa. Jambo la tano nilitegemea kusikia kuwa walikula. La hasha hawakula ule mkate. Aya ya 31 inasema macho yao yakafumbuka. Alifanya mambo 4 tu kati ya mambo matano. Hebu fikiria mtu aliyekufa, mara ghafla unamuona ukiwa naye mezani baada ya kubariki chakula, hakika hautakula chakula hicho. Ni hakika Vijana wale wawili hawakula chakula kile baada ya macho kufumbuliwa bali walitoka mbio kurudi Yerusalemu.

Kwa nini Yesu hakuwafumbua macho yao wale vijana wawili? Kwa nini aliwafumbua macho yao mara baada ya mafundisho ya muda mrefu? Kwa nini hakuwafumbua macho yao katikati ya  njia? Yesu hakuwafumbua macho yao kwa sababu hataki kanisa lake kwenda kwa MISUSUMIKO. Yesu anataka kanisa liende kwa maandiko ya Mungu. Anataka kanisa linalosoma maandiko ya Mungu. Wanaosoma neno la Mungu watafumbuliwa macho yao. Wanaosubiri kuja kwa Yesu kwa mara ya pili ni wale kila siku wanasoma maandiko matakatifu.

La muhimu ni neno la Mungu ndani ya mioyo yetu. Kumjua Mungu kutakamilishwa na neno la Mungu kukaa ndani ya mioyo yetu ili kuzaa nia njema ya kumwabudu Mungu. Torati ya neno la Mungu ikae ndani yetu.

BWANA AWABARIKI

JIANDAE KUKUTANA NA YESU KATIKA MAKAMBI 2017

Written By SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH on Monday, July 17, 2017 | July 17, 2017

Mchungaji Simeo Makunja- Mkurugenzi wa Kaya na Familia na Katibu wa Wachungaji wa Jimbo la Nyanza Kusini

 Mkurugenzi kutoka Jimbo la Nyanza Kusini anayesimamia masuala ya Kaya na Familia ambaye pia ni Katibu wa Wachungaji wa Jimbo amesema kuwa Yesu Kristo alikuwepo toka mwanzo wa uumbaji wa Dunia, kwa hiyo wanadamu wote wasikatae mafundisho ya Yesu ili wapate hekima. "Ana heri mtu asikiaye neno la Mungu naye atapata kibali mbele za Mungu. Na kila achukiaye hekima ya Mungu anakaribisha mauti na kupotea milele". Amesema Mchungaji Makunja.

Mchungaji Makunja amesema hayo wakati wa usiku akifundisha neno la Mungu katika kipindi cha "Wazo la Usiku". Akinukuu maneno katika kitabu cha Yohana 1:14 amesema kuwa kupitia Yesu Kristo, Mungu wa Mbinguni amejifunua na sasa sio siri. Kupitia Yesu Kristo ukombozi wa mwanadamu ulitimia na kumfanya mwanadamu awe huru katika uchaguzi wa kumtumikia Mungu au Shetani.

Pia Mchungaji Makunja amemuelezea Yesu Kristo Ni Mungu ambaye kupitia kwake kila kiumbe chenye uhai na visivyo hai viliumbwa kupitia kwake na kupitia kwake Yesu Kristo, Upendo wa Mungu umeonekana kupitia Kifo cha Yesu.

Mchungaji Makunja ametoa wito wa kuhudhuria sikukuu ya vibanda ili kila atakayehudhuria apate hekima ya Yesu Kristo na kuweza kupata kibali katika Ufalme wake ambao ameenda kuundaa mbinguni. Amesema uamuzi wa Yesu Kristo kufanyika Mwanadamu ilikuwa na kusudi la Kuumba na ukombozi wa Mwanadamu ili mwanadamu aweze kumwabudu na Kumsuduju Yesu Kristo (Ufunuo 13:8-9). "Tunapokuja hapa kwenye makambi, tunakuja kutafuta hekima na kuweza kumwabudu Yesu wetu ambaye ndiye Mungu wetu".


 
Need Support? Contact : Creating Website and Blog | Stanley Isaac Manyonyi | Twitter
Copyright © 2017. SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger