Home » » MCHUNGAJI BUTOKE AONGOZA UFYATUAJI MATOFALI YA GHARAMA NAFUU

MCHUNGAJI BUTOKE AONGOZA UFYATUAJI MATOFALI YA GHARAMA NAFUU

Written By SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH on Monday, April 10, 2017 | April 10, 2017

Mwenyekiti wa Jimbo la Kusini mwa ziwa Viktoria Mchungaji Sadock Butoke  ameongoza wanasemina kutoka sehemu mbalimbali za jimbo la kusini mwa ziwa Viktoria kufyatua matofali yanayotokana na udongo na saruji. 

Mkufunzi kutoka shule ya Waadventista Alpha iliyopo Kigoma, ndugu Kulu Jeremiah Mahwago alifundisha wanasemina faida ya kutumia matofali yanayotokana na udongo na saruji. Mojawapo ya faida ya matofali haya ni rafiki kwa mazingira kwa sababu hayahitaji matumizi ya nishati ya moto kama vile kuni kuyachoma. 

Pia mkufunzi alikaririwa akisema katika ujenzi hutumia mfumo wa kupachika bila kutumia saruji au udongo. Mara baada ya kupachika na kufika katika hatua ya madirisha ndipo mjenzi atalaimika kutumia saruji kwa lengo la kufunga renta.

Wakati wa kuweka mfumo wa umeme na maji, uvunjaji wa tofauti hautakuwepo kwa sababu tofali hizi zilizotengenezwa kwa saruji na udongo, zina matundu katikati ambayo hutumika kupitisha mfumo wa umeme na maji.

Uhai wa tofali hizi unategemea maji kwa siku 28 na hazitumii jua kukaushwa bali baada ya kufyatuliwa zinahitaji kivuli maana zinakauka kwa kutegemea upepo.

Mchungaji wa mtaa wa Shinyanga Mjini, mchungaji Kilinda J.J anashukuru uongozi wa jimbo la kusini mwa ziwa Victoria kuleta semina katika eneo la Ndala- Shinyanga. Amesema kuwa semina hii imewasaidia vijana wa kanisa kupata ujuzi wa kutengeneza matofali yatokanayo na saruji na udongo, kwa hiyo anaamini baada ya semina hii vijana watarudi katika maeneo yao na kuanza kujiajiri. Pia vijana wataweza kujenga nyumba makazi yao kwa gharama nafuu.

Mchungaji Kilinda aliendelea kusema kuwa semina hii italeta matokeo chanya ya kuhakikisha ujenzi wa shule ya sekondari ya Shinyanga (Shinyanga Adventist Secondary School) unakamilika ili kuweza kutoa huduma ya elimu kwa jamii ya watanzania. Matofali yatakayotengenezwa yatatumika kujenga jengo la utawala lenye ofisi ya mkuu wa shule, ofisi ya makamu wa mkuu wa shule, ofisi ya walimu na stoo.

Wakati huo huo mkurugenzi wa elimu na uhuru wa dini wa jimbo la kusini mwa ziwa Victoria mwalimu Isaacks Manyonyi amesema Shinyanga Adventist Secondary School itaanza Januari 2018 na kuwaomba wadau wote wa elimu kutoa misaada ya hali na mali ili kuweza kukamilisha ujenzi wa shule hii.

Semina hii imeanza tarehe 10-13 April 2017


               
Share this article :

Post a Comment

 
Need Support? Contact : Creating Website and Blog | Stanley Isaac Manyonyi | Twitter
Copyright © 2017. SHINYANGA CENTRAL SDA CHURCH - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger